Nguu za Jadi - Mtindo wa uandishi

 MTINDO WA UANDISHI

Mbinu Za Sanaa

Taharuki

Hadithi inapoanza, Mangwasha na wanawe wako kanisani. Kuna jambo ambalo limekumba eneo nzima la Matango ambalo wasomaji hawana habari ni jambo gani. Wanawe Mangwashwa hawana taarifa kuhusu aliko baba yao, na wasornaji hawajui ni kitu gani kimetokea, hata mumewe Mangwasha kumwachia wanawe na umaskini (uk. 1). Wasomaji analazimika kuendelea kusoma ili kupata majibu ya maswali haya.

Hadithi ndani ya hadithi

Hadithi ndani ya hadithi ni hadithi au kisa ambacho husimuliwa ndani ya kisa au hadithi kuu. Mara nyingi, hadithi ndani ya hadithi hutumiwa kuelezea jambo fulani ambalo kwa namna fulani linahusiana na kisa kikuu kinachosimuliwa.

Sauni anawasimulia marafiki zake, wakiwa nyumbani kwa Lonare, kisa cha mwanamke fulani ambaye alidhani alishabihiana sana na Sihaba (uk. 81).

Taswira

Taswira ni picha ambazo hujengeka akilini mwa msomaji wa kazi za kifasihi. Taswira anazopata msomaji wa Nguu za Jadi ni nyingi, miongoni mwake:

Kuna taswira ya Mangwasha akivikagua vifurushi vya nguo na vitu vingine vichache alivyoweza kuokoa visichomeke (uk. 2). Taswira hii inakuza maudhui ya umaskini na hali ya uhitaji.  

Jazanda

 Anwani ya riwaya hii ni ya kijazanda. Nguu ni kilele au upeo wa mlima. Kitamathali, nguu ni vikwazo au matatizo ya ainati yanayokwamiza maendeleo ya kijamii, kama vile ukabila, unyanyasaji wa wanawake, ubabedume, uongozi mbaya, umaskini, ukosefu wa ajira, ufisadi, na kadhalika.

Mtemi Lesulia analinganishwa na mjusikafiri. Kitendo cha mjusikafiri kuingia kwenye shimo huku akiotea chakula cha mchwa, sawa na mchwa wenyewe, ni jazanda ya uongozi mbaya.

Mchwa ni wananchi wa kawaida, nao viongozi, kama vile Mtemi Lesulia, ni mjusikafiri ambao wanafakamia kila kitu, kiasi kwamba wananchi wa kawaida wanabaki katika dhiki kubwa (uk. 93).

Kinaya

Ni kinaya kwamba watu wasiokuwa na elimu ya kutosha ndio wanaopata kazi katika nchi ya Matuo huku watu wengi waliohitimu vizuri, hasa wa kabila la Waketwa, wakiwa hawana kazi (uk. 44).

Ni kinaya kwamba Mtemi Lesulia hataki kuachilia kiti cha utemi ilhali ni wazi kwamba uongozi wake umeiingiza nchi katika hali ya uhitaji, umaskini uliokithiri na hali ya maadili. 

Mbinu za Lugha/TamathaIi za Usemi

Sitiari

Mbungulu anamwambia Mangwasha kwamba amwepuke Sagilu sana kwani yeye ni 'moto wa kuotea mbali' (uk. 79). Hii ina maana kwamba Sagilu ni mtu hatari sana au mwovu.

Mangwasha anamwambia Mbungulu kwamba "...Sagilu ni chua ndani ya mchele lakini wakati mwingine hufanana na huo huo mchele..." (uk. 80), kumaanisha kuwa Sagilu ni kigeugeu, ni mtu hatari huku wakatiwingine akijifanya mtu mzuri.

Tashbihi

Tashbihi pia huitwa tashbiha au mshabaha. Katika mbinu hii, mwandishi hufananisha kitu kimoja na kingine. Baadhi ya maneno yanayotumiwa kufananisha huwa kama, mfano wa, sawa na, na mithili ya.

Zifuatazo ni baadhi tu ya tashbihi zilizotumiwa katika riwaya ya Nguu za Jadi, kwani ni nyingi sana kitabuni."...Amsahau kama vile mtoto anavyolisahau titi la mamaye..." (uk.1): Mangwasha anawazia kumsahau mumewe kabisa. "Huku macho yakiangaza kama anayesaka hirizi iliyopotea..." (uk 3) kama mtu anayetafuta kitu muhimu sana bila mpangilio au utaratibu wowote.  

"Mwishowe, (Mrima) alisalia kimya mithili ya kondoo aliyekuwa akipelekwa machinjioni..." (uk. 115) kumaanisha Mrima alitulia kabisa.

Tashihisi/uhaishaji

Tashihisi pia huitwa uhaishaji au uhuishi. Hii ni mbinu ambapo kitu kisicho na uhai hupewasifa za binadamu.

Methali

Methali ni usemi mfupi, wenye maana pana, busara au hekima ulio na mizizi katika jamii fulani na unaelimisha, kuasa au kukejeli watu au vitendo fulani katika jamii lakini kwa njia iliyofumbwa na kuwekewa tasfida. Hivyo basi, jamii tofauti zina methali tofauti kuambatana na tamaduni na mila zilizomo. Zifuatazo ni baadhi ya methali zilizotumiwa riwayani na maana zake kimuktadha, "...chakani mwa simba halali nguruwe..." (uk. 6) hii inarejelea uhusiano wa chuki kati ya Wakule na Waketwa.

• "...Heri nusu ya shari kuliko shari kamili..." (uk. 13) methali hii inarejelea hali ya Mangwasha kuona ugumu kumweleza Lonare matatizo yake, hasa ikizingatiwa kwamba yeye ni mwanamke.  

• Sagilu anamwambia Mrima, "...nahodha kamwe haogopi mawimbi..." (uk. 19) kama njia ya kumtisha kuhusu uhusiano wake na Mangwasha kwani Sagilu anamtaka Mangwasha kimapenzi. Kauli "...nahodha kamwe haogopi mawimbi... " inatokana na methali "Nahodha hodari hachelei dhoruba".  

• Mrima anamwambia Sagilu, "...kaa ukijua kwamba ghadhabu ya bahari ni furaha ya papa..." (uk. 19) kumaanisha kwamba yeye haogopi vitisho vya Sagilu.  

Maswali ya balagha

Maswali ya balagha ni mbinu ambapo mwandishi hutumia maswali yasiyohitaji majibu. Lengo la maswali haya ni kumfanya aliyeulizwa ajisake na ajikosoe au ajifikirishe. Wakati mwingine, maswali ya balagha huwa yanakusudiwa kukejeli.

Yafuatayo ni baadhi ya maswali ya balagha yaliyotumiwa riwayani na maelezo kuyahusu.

Starehe ya usingizi itoke wapi ikiwa vurumai na mahangaiko yale yalimwacha fukara? (uk.1) kumaanisha kwamba hali ya zogo na mahangaiko ilimkosesha usingizi.

• Lakini...lakini hata akikitegua, salama itoke wapi? (uk. 1) kumaanisha kwamba hata kama angejua alikokuwa mumewe, haingesaidia chochote kwani mumewe alikuwa tayari keshamwachia madhila mengi.

• Barua ile ina maana gani kwake sasa hata akiisoma? (uk. 3). Mangwasha anashangaa barua anayopata itasaidia nini kwani mumewe hayupo karibu kumsaidia katika hali yake.

• Kuna mtu akaiba mali yake mwenyewe ya kumhifadhi baadaye? (uk. 47). Mangashwa anaajabia hali ya nchi ya Matuo kuwa na watu ambao wako mbioni kuifilisi nchi bila kuwazia kesho yao.

Misemo na nahau

Hakupata hata lepe la usingizi (uk. 1), kumaanisha Mangwasha hakuweza kulala hata kidogo. Mrima wake keshaonjeshwa asali, sasa yu radhi kuchonga mzinga (uk. 37), kumaanisha kwamba Mrima ameshashawishiwa kabisa kwa pesa, na sasa hata familia haijali tena.

Mabepari wachache wakaanza kuhodhi vyakula na kuviuza kwa bei ya dhahabu (uk. 45), kumaanishaa wakaanza kuviuza kwa bei ya juu sana.

Mwamba alitia masikio pamba, akaendelea na kampeni zake (uk. 53), kumaanisha Mwamba alipuuza masuto ya Sagilu.

Bila shaka tutajua mbivu na mbichi kuhusu mkasa ute (uk. 73), kumaanisha tutajua ukweli wote kuhusu mkasa huo.

Chuku

Chuku ni mbinu ambayo huhusisha kutilia kauli au habari chumvi ili kuleta msisitizo. Mbinu hii imetumiwa ifuatavyo:

Baada ya Lonare kushinda uchaguzi, tunaambiwa kwamba watu wanasakata densi na kuvimba miguu kama walioshikwa na ugonjwa wa matende (uk. 177), kumaanisha kwamba walisherehekea kwa msisimko mkubwa.

Mbungulu anamwambia Mangwasha kwamba Mrima amekonda kiasi kwamba akipuliziwa pumzi ataanguka (uk. 97), kumaanisha kwamba Mrima amekonda sana.

Mwandishi anasema kwamba eneo la Matango lilikuwa kichaka kikavu kilichohamwa hata na panya (uk. 65), kumaanisha eneo hilo lilionekana kama ambalo halikuwa na faida.  

Mrima anasema kwamba Sagilu aliwahi kuwa na masuria (vimada) watoshao kijiji kizima (uk. 18), kumaanisha kwamba Sagilu alikuwa na vimada wengi sana.

Dhihaka/Kejeli/Stihizai

Chifu Mshabaha anamdhihaki Mangwasha anapomwambia, "Toka mbele yangu. Kwenda!

Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba..." (uk. 20). Chifu huyu anaudhika kwa sababu

Mangwasha amemkataa Sagilu na anaelekea kuolewa na Mrima, ambaye hana mali.

Sagilu anamdhihaki Mangwasha anapomuuliza kama hajachoka kulisha na kuvisha mtu asiye na be wala te (uk. 102) kisha anamuuliza kwa nini hataki kujibu swali muhimu kama lile. Bila shaka, Sagilu anajua kwamba anamuudhi Mangwasha.

Dhihaka inajitokeza pale tunapoambiwa, "...Ngoswe alikenua meno akatoa kicheko ghafla.

Papachi kinywani zikicheka pamoja naye..." (uk. 133) kumaanisha kwamba Ngoswe hakupendeza kutokana na papachi kinywani mwake.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

Nguu za Jadi - Sifa na umuhimu wa wahusika

Nguu za Jadi - Madhari katika riwaya

Nguu za jadi - Muhtasari wa Matukio Katika Riwaya