Nguu za Jadi - Madhari katika riwaya

 MANDHARI KATIKA RIWAYA

Mandhari katika fasihi ni muktadha au mazingira ambayo hadithi au kazi ya fasihi inasimikwa. Ni maelezo ya mahali, wakati, hali ya hewa, utamaduni, na mambo mengine yanayotoa mazingira ya kazi za fasihi. Mandhari husaidia kutoa msukumo kwa hadithi na kuwapa wasomaji au wasikilizaji taswira ya kina na hisia ya mazingira ambayo hadithi inatendeka.

Mandhari katika fasihi inaweza kuwa ya kibinadamu, kisiasa, kijamii, kijiografia, au hata kisiasa. Kwa mfano, mandhari inaweza kuwa jangwa lenye joto kali, mji mdogo wa vijijini, mazingira ya mijini, au hata anga la kisiasa lenye migogoro na yote yaibue masuala tofauti.

Kwa kifupi, mandhari katika fasihi ni muktadha au mazingira ambayo hadithi au kazi ya fasihi inafanyika, na inachangia kujenga hisia ya kweli na kutoa msukumo wa kina kwa hadithi au kazi.

Mandhari hurejelea mahali,wakati na hali ambamo ya kazi ya kifasihi hutukia. Katika riwaya ya

Riwaya ya Nguu za Jadi imejikita katika mandhari anuwai, kuna kanisani walimotorokea wakimbizi, nyumbani kwa Mangwasha, Kanisa la Mtakatifu Marko kulikofanyika arusi, Majaani, Ponda Mali, Mkahawa wa Saturn, Ofisi ya Chifu Mshabaha, Nyumbani kwa Sagilu, miongoni mwa mengine. Mandhari hayo yameanishwa ifuatavyo:

 

KANISANI-WAKIMBIZI WALIPOTOROKEA

Hapa ni pale ambapo Mangwasha pamoja na wakazi wengine wa Matango walikimbilia baada ya makazi yao kuteketezwa usiku.

i. Yametumika kujenga maudhui ya ukatili. Wenyeji wa –la Matango wamekesha pale kanisani  baada ya kuchomewa makao yao.

ii. Yanachimuza  maudhui ya utetezi wa haki. Lonare anafika pale kanisani siku inayofuta baada ya mkasa wa kuchomewa makao na kuwaeleza  wenyeji wa Matango lazima wangpigania kilicho chao.(uk 65)

iii. Yanadhihirisha matatizo  yanayowakumba wakimbizi.  Baadhi ya waliofika pale walilala ardhini.  Mangwasha aliwatazama akina mama walivyojikunyata na vitoto vyao kutokana na kibaridi cha  alfajiri.

iv. Yanaonyesha wakati ambapo wenyeji wa Matango walichomewa makazi yao.  Wanawake waliokuwa wakitoka kwenye biashara zao waliwaona vijana  waliobeba mageleni tupu yalionuka mafuta ya petroli.

v. Yanachimuza maudhui ya ukatili.  Vijana waliokuwa wamebeba mageleni yale waliingia katika gari jekundu na sauti ya mwanamke ikasikika ikiwauliza kama walikuwa wamekamilisha kazi.

vi. Yanajenga maudhui ya ufisadi.   Tunaelezewa na mwandishi kuwa Mbwashu alishirikiana na vigogo wengine matajiri kufisidi pato la nchi. Aliagiza bidhaa kutoka nje bila kulipa ushuru.

vii. Yanaonyesha matumizi mabaya ya mali ya umma.  Mbwashu anafika katika eneo lile akibebwa na gari aina ya Land Rover liliominiwa kuwa la polisi na hana wadhifa wowote serikalini.

viii. Yanajenga sifa za mbungulu kama mwenye busara. Anasema magari mekundu ni mengi na ya aina moja hivyo bila kujua nambari zake wangekuwa  wakifanya kazi bure.

ix. Yanajenga mtindo wa ri waya kupitia mbinu mbalimbali kama vile Mazungumzo ya  Mkurugenzi wa Ardhi, Lonare na Sauni.

x. Yanachimuza maudhui ya unafiki. Nanzia anafika eneo lile kutoa msaada wake ilhali anajua arhi ile ingemfaidi yeye na Mbwashu.

xi. Yanachora vijana kama wasio na utu.  Wanatumiwa katika kuwachomea wenyeji wa Matango makazi yao.

xii. Yanajenga sifa za Lonare kama mwajibikaji.  Baada ya kujua kuwa wafuasi wake wamekimbilia pale kanisani anawaleta askari ambao wangewalinda.

xiii. Yanamjenga Mwangasha kama mchapakazi. Mwandishi anasema kuwa Chifu Mshabaha angelimpiga Mangwasha kalamu lakini alijua hakuna mwengine ambaye angeweza kuteleleza majukumu mengi kwa pamoja bila kulalama.( uk 69).

xiv. Yanaonyesha maudhui ya uwajibikaji.  Serikali inawaletea waliochomewa nymba zao mahema, chakula na maji.

xv. Yanajenga ploti kwa kuonyesha usuli wa uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia.  Waketwa wanachomewa makao yao ili ardhi yao ya Matango ichukuliwe.

xvi. Yanajenga ploti kwa kuonyesha upeo wa mgogoro    baina ya wenyeji wa Matango na uongozi wa Mtemi Lesulia pale anapowatumia wenzake kuchoma makao ya Wanamatango.

xvii. Kukimbilia kwa wenyeji wa Matango hapa kanisani ni kipenglele cha ploti.  Inatumika kuonyesha upungufu wa utu wa binadamu kiasi cha kuachomea makazi yao.

 

 

 

KANISA LA MTAKATIFU MARKO ARUSI ILIKOFANYIKA

Hapa ndipo arusi ya Mrima na Mangwasha ilifanyika.

i. Yanachimuza maudhui ya mapenzi. Mangwasha na Mrima wanapendana na kufanya arusi yao katika kanisa hili.

ii. Kuonyesha maudhui ya uwajibikaji.  Waliohudhuria harusi hii wanawajibika kwa kuwaletea maarusi zawadi.

iii. Yanajenga maudhui ya ukatili. Sihaba anatumiwa kutaka kuharibu arui kwa kutumia kilipuzi.

iv. Yanajenga sifa za Mrima kama mwenye tahadhari. Anamtumia msimamizi wao ili amzuie Sihaba kuwadhuru.

v. Yanachimuza maudhui ya utabaka. Baada ya kilipuzi kulipuka  kuna wale wanaoingia kwenye magari yao na wengine waliopiga mbio hadi mahali salama.

vi. Yanajenga mgogoro baina ya msimamizi na Sihaba anapomzuia kupita wapeleka zawadi yake.

vii. Yanajenga ploti kutokana na msimamizi kutupa kifurushi alichokuja nacho Sihaba na kusababisha kutibuliwa kwa harusi. Taharuki injengeka kwa msomaji.

 

MANDHARI YA MAENEO YA PONDA MALI

a) Kukuza athari za ulevi – Mrima analewa kupindukia na kuisahau familia yake.

b) Kukuza utowajibika – Mrima anakosa kuwajibikia mahitaji ya familia yake na kufika Ponda Mali Kulewa.

c) Kuonyesha uozo katika jamii- walevi wanalewa kupindukia.

d) Kukuza sifa ya Mrima – kuwa mlevi na mtelekezaji majukumu.

e) Kukuza sifa ya Mrima – kuwa asiyewajibika –Mrima hakuwajibikia familia yake anapoenda Ponda Mali kulewa.

f) Kukuza sifa ya Mangwasha – kuwa mwajibikaji-aliwajibika kufika ponda mali kumtafuta mumewe.

g) Kukuza mbinu za mtindo– (majazi) ponda mali ni jina la kimajazi.

 

MANDHARI YA MAJAANI:

Maeneo ambapo mrima alikuwa ametorokea.

i) Kupitia mandhari ya Majaani, tunaona athari za uongozi mbaya.

ii) Wananchi wanakosa mahitaji ya lazima na kunyang'anyana vyakula na kunguru.

iii) Yanaendeleza maudhui ya utabaka. Walisitiriwa na makombo ya vyakula kutoka katika jaa hili kuu.    

iv) Kupitia mandhari haya ndipo tunapojua alipopotelea Mrima.

v) Kupitia mandhari haya, athari za kuwa mtu rahisi kushawishika zinabainika. Mrima anaishia kufutwa kazi kutokana na ulevi baada ya kushawishiwa na Sagilu.

vi) Kupitia mandhari haya, sifa ya Mrima inabainika kuwa mtu aliyekengeuka. Anaishia kuishi Majaani kutokana na ulevi.

vii) Maudhui ya uchafuzi wa mazingira yanabainika kupitia mandhari haya. Ni katika eneo hili ndipo takataka zote za mji zilitupwa.

viii) Mandhari haya yanamsawiri Mangwasha kuwa mwenye mapenzi ya dhati. Anaenda kumtafuta mumewe ili kumvua kutoka jaa hilo la ulevi.

ix) Ushikamano wa kijamii unabainika kupitia mandhari haya. Mbungulu, Lonare na wengine wanaenda kumtafuta hapo.

x) Mandhari haya yametumiwa kuonyesha jinsi Mangwasha anavyovunja nguu za jadi. Anataka

kwenda kumtafuta mumewe Majaani hata ikiwa angeenda peke yake licha ya jadi ya mke kutomtafuta mumewe.

xi) Mandhari haya yanaendeleza ploti kwa kuendeleza mgogoro kati ya Mangwasha na Sagilu. Sagilu ndiye chanzo cha Mrima kuwa Majaani.

xii) Kujenga sifa ya Mrima – kuwa mlevi, alilewa kupindukia hadi akapumbaa

xiii) Kujenga mtindo(majazi) – majaani-kulikotupwa kila kitu.

xiv) Kujenga mtindo(taswira) – taswira ya mji huu jinsi uliuwa mchafu jinsi watoto wa mtaa ni wachafu, jinsi Mrima alisifia majaani akiwa mchafu.

xv) Kuonyesha umaskini-watoto wa mtaani wanafika hapa kula mabaki ya kilichotupwa.

xvi) Kuonyesha utabaka -vijana waliofika hapa ni wa tabaka la chini.

xvii) Ukuonyesha uajibikaji – alipomkosa Mrima ponda mali, Mangwasha alienda  Majaani kumtafuta.

xviii) Kuonyesha madhila katika jamii- kuna watoto wa mitaani ambao hawana mwokozi.

xix) Uongozi mbaya – viongozi hawajawajibika kuwaokoa watoto wa mitaani kutokana na uharibifu huku.

 

NYUMBANI KWA MANGWASHA

i. Yanajenga maudhui ya uwajibikaji.  Mangwasha analea watoto wao pekee mumewe anapotorokea ulevini.

ii. Yanajenga ploti kutokana na matendo yanayofanyika nyumbani humu kama vile   bahasha anayopewa Mrima ili kumsaidia Mtemi Lesulia katika kampeni zake.

iii. Yanaonyesha changamoto zinazokumba asasi ya ndoa.  Mrima anatelekeza majukumu ya familia na kugeukia ulevini.

iv. Yanaendeleza maudhui ya mapenzi.  Mangwasha  anatumia lugha ya kimapenzi anapoongea na mumewe.  Kwa mfano anamwita my love (uk 41)

v. Yanajenga sifa za Mangwasha kama mwajibikaji.  Yeye ndiye amebaki kukidhi mahitaji ya wanawe baada ya mumewe kutoroka.

vi. Yanadhihirisha kutowajibika kwa Mrima.  Hajakuwa kakijishughulisha na mahitji ya familia yake kama vile chakulam mavazi n.k.

vii. Yanaendeleza maudhui ya ukatili.  Lonare anapopotea kabla ya uchaguzi anapatikana nje ya nyumba ya Mrima akiwa hali mahututi.

viii. Yanakuza maudhui ya ufisadi. Mangwasha anamwambia Sagilu kuwa anawazuzua wasichana kwa pesa.

ix. Yanajenga maudhui ya malezi.  Mangwasha anawalea sayore na Kajewa baada ya mumewe kutoroka.

x. Yanajenga maudhui ya utabaka. Sagilu anapomtembelea Mangwasha anamwambia alitaka aishi katika makasri yanayolindwa na majeshi na askari badal ya kuishi kwenye mapango.

xi. Yanachimuza sifa za Mrima kama mbabedume. Anamwambia mkewe kuwa hawezi kumzuia kuoa mke mwingine. (uk41)

xii. Yanajenga maudhui ya elimu. Sayore alihitajika kurudi shuleni na vitabu vipya kama wenzake.

xiii. Yanajenga ploti kupitia maswala yanayoibuliwa kama vile mgogoro baina ya Mangwasha na Sagilu anayemtka kimapenzi.

xiv. Yametumika kuonyesha athari za ulevi kutikana na ulevi, Mrima ameshindwa kutekeleza majukumu yake nyumbani.

xv. Ynajenga maudhui ya utamaduni. Mrima anasema kuwa wanawake wa sasa wanavunja kila mwiko uliowekwa na wazee.  Anamuuliza mkewe toka lini mwanamke akamuuliza mumewe kule aendako au atokako.

xvi. Yanadhihirisha nafasi ya mwanamke katika jamii inayozungumziwa.  Mrima anasema kuwa mwanamke akishailewa azae na kutumikia jamaa yake bila kuulizauliza maswali.

xvii. Yanamsawiri Mangwasha kama aliyezinduka.  Anasema kuwa baadhi ya tamaduni ambzo Mrima anaishi kumkumbusha zimepitwa na wakati.

xviii. Yanajenga sifa za Mangwasha kama mwenye kujithamini.  Anapoletewa bahasha yenye pesa na Sagilu ili amkubalie mapenzi anaikataa na kumrushis. ( uk 60)

xix. Yanajenga mtindo kupitia mbinu kama vile mazungumzo baina ya Mangwasha na Sagilu.

xx. Yanajenga sifa ya Sagilu kama mwenye taasubi ya kiume.  Anasema kwamba hajawahi kukataliwa na mwanamke yeyote.  Hivyo Mangwasha hangemshinda. (uk 60)

 

 

 

 

BECKON ACADEMY

Walikosomea Lombo na Mashauri

i. Yanachimuza matatizo yanayokumba watoto mayatima.  Una kijana anayesemekana kuwa na ugonjwa wa chawa.

ii. Yanazua mgogoro baina ya wenye mamlaka na wapinzani. Mashauri anasema ndio sasa tunataka kubadilisha uongozi kusiwe na mtoto yatima wala tabaka la juu.

iii. Yanakuza nafasi ya wahisani waliomleta shuleni Beckon Academy kwa sababu ya uerevu wake.

iv. Yanaonyesha utepetevu wa serikali.  Serikali haishughulikii hali ya kijana huyo yatima ambaye ana ugonjwa wa chawa.

v. Yanajenga maudhui ya umaskini.  Ugonjwa wa chawa na uchafu wa kijana huyu yatima ni  ishara ya umaskini.

vi. Yanajenga sifa za Mashauri kama mwoga.  Aliambiwa na mwalimu ashike nyoka akidhani yu hai akatoroka shule siku mbili.

vii. Yanakuza maudhui ya elimu. Hapa ndipo Lombo na Mashauri walisomea hadi kidato cha nne.

 

MANDHARI YA NYUMBANI KWA MBUNGULU

a) Kuonyesha ukarimu wa Mbungulu-Mangwasha anapofika kwake anamkaribishwa kwa kikombe cha chai.

b) Yanaendeleza uwajibikaji wa marehemu mumewe Mbungulu ambaye akiwa hai alimtimizia mkewe mahitaji yote.

c) Yanakuza urafiki- Maangwasha alifika kumtembelea rafikiye Mbugulu kwa kuwa ni marafiki.

d) Ushauri mwema – Mbugulu anamshauri Mangwasha vyema kuhusiana na suala lake.

e) Nafasi ya mwanamke – mwanamke ni mshauri mwema – Mbugulu anamshauri Mangwasha jinsi ya kukabiliana na Mrima.

 

MANDHARI YA HOSPITALINI

Hospitalini alipolazwa Sagilu mjini Taria.

i. Yanajenga mtindo wa riwaya kupitia mbinu ya mazungumzo baina ya Mashauri na Lombo.

ii. Yanaonyesha maudhui ya msamaha.  Sagilu anaomba wote aliowakosea msamaha.

iii. Yanajenga sifa za Mashauri kama mwajibikaji.  Anakuja kumwona Sagilu hospitalini.

iv. Yanajenga maudhui ya majuto.  Sagilu anajutia uovu wake.

v. Yametumiwa   kujenga dhamira ya mwandishi.  Mwandishi anaonyesha kuwa hatima ya maovu ni maangamizi.  Mali ya Sagilu inatwaliwa na serikali.

vi. Yanajenga maudhui ya ufisadi. Mali aliyomiliki Sagilu haikuwa yake bali alipata kwa njia haramu.  Serikali inatwaa mali hiyo.

vii. Yanaendeleza maudhui ya utamaduni. Sagilu anaenda Munyuni kutakaswa kutokana na mwiko aliovunja.

 

Hospitalini alipolazwa Lonare.

i. Yanajenga maudhui ya ukatili.  Lonare anamtajia Ngoswe kuhusu biashara yake ya ulanguzi wa dawa za kulevya zinazodhuru vijana wa shule.

ii. Yanajenga sifa za Ngoswe kama mlanguzi wa dawa za kulevya.  Amekuwa akifanya biashara ya kulangua dawa za kulevya na kuziuza hata shuleni.

iii. Yanawajenga Lombwe na Mashauri kama wawajibikaji. Walisalia hospitali kumchunga Lonare hadi pale alipoweza kuongea.

iv. Yanajenga mtindo wa riwaya kupitia mbinu ya mazungumzo yanayobadilisha mtindo wa riwaya wa masimulizi.

v. Yanadhihirisha uozo uliopo katika jamii.  Ngoswe anauzia vijana wa shule dawa za kulevya bila kujali.

vi. Yanaonyesha maudhui ya mabadiliko. Ngoswe anamhakikishia Lonare mbele ya Lombo na Mashauri kuwa angebadili mwenendo wake.

Hospitalini anapolazwa Nanzia

i. Yanajenga ploti kutokana na ujumbe anaopewa Ngoswe na mamake Nanzia kuwa Mtemi Lesulia si baba yake.

ii. Yanajenga maudhui ya kifo/tanzia. Baada ya Nanzia kusema na Ngoswe anaaga dunia.

iii. Yanajenga sifa za Nanzia kama mzinifu.  Anamfahamisha Ngoswe kuwa Lesulia si babake bali Sagilu ndiye babake.

iv. Yanadhihirisha umuhimu wa jamaa na marafiki.  Ngoswe anawapata babake na marafiki wa Nanzia pale hospitalini.  

v. Yanakuza dhamira ya mwandishi.  Mwandishi anaonyesha tamati ya maovu ni dhiki na kifo.

 

MANDHARI YA MKAHAWA WA SATURN

a) Kuonyesha wajibikaji – Mashauri anawajibikia kwa kumfuata Sagilu mkahawani alivyoshauriwa na rafikiye Ngoswe.

b) Kuchimuza maudhui ya ajira na kazi – wahudumu walifanya kazi ya kuwahudumia wateja katika mkahawa huu.

c) Kujenga sifa za Sagilu – kuwa mwenye tamaa ya mapenzi anafanya mapenzi na Cheiya kutokana na tamaa yake.

d) Kujenga mtiririko wa matukio katika riwaya – njama ya Lesulia na Sagilu kumhonga Mrima inafichuka hapa mkahawani, Sagilu aligombana na Masahauri, Ngoswe alimwita Sagilu ili washauriane papa hapa.

e) Yanakuza siasa – mikutano ya siasa ilifanyika hapa mkahawani humu.

f) Ufisadi – Lesulia na Sagilu walikuwa wamemhonga Mrima ili ampinge Lonare, njama hi ilitibuka humu mkahawani akina Lonare walipofika pale kurudisha pesa ambazo Mrima alipewa na Sagilu.

g) Usaliti – Cheiya anamsaliti Mashauri kwa kufanya Mapenzi na Sailu katika mkahawa huu.

h) Uzinzi – Cheiya na Sagilu wazini katika mkahawa huu.

i) Tamaa- Sagilu ana tamaa ya mpenzi na hata hajali heshima wala utamaduni. Ndiyo sababu anajamiiana na mpenzi wa mwanawe.

 

MANDHARI YA NYUMBANI KWA SAGILU

i. Yanajenga ploti kwa kuwatambulisha wahusika wengine na matendo yao katika riwaya.  Sagilu anadokeza kuwa Ngoswe ana ndugu mwingine aitwaye Mdando aliyekaa Ulaya na pia anamtambulisha Mzee Lengima ambaye ni mzaziwe Sagilu/babuye Ngoswe.

ii. Yanajenga sifa za Nanzia kama mzinifu/mkware.  Sagilu anaeleza jinsi Nanzia alijihusisha na mapenzi na mhindi mfanyabiashara.

iii. Yanaonyesha changamoto zinazoikumba asasi ya ndoa. Lesulia na Nanzia wekaa kwa muda mrefu bila kupata mtoto.

iv. Yanamchora Nanzia kama mwongo. Ameishi kumdanganya Ngoswe kuwa Mdando anasoma ulaya na kuwa akimaliza angerudi.

v. Yanajenga sifa za Sagilu kama mzinifu.  Kujihusisha na mapenzi na Nanzia ni kitendo cha kuzini kwani tunajua ana mke.

vi. Yanajenga mtindo wa rewaya kupitia mbinu ya mazungumzo baina ya Sagilu na Ngoswe yanayobadilisha mtindo wa usimulizi uliotumika kwa wingi.

 

 

MANDHARI YA RED BEADS LODGINGS

i. Yanaendeleza ukiushi wa haki za watoto.  Wazazi wanawaingiza watoto wao wasichana kwnye ukahaba.

ii. Yanaendeleza maudhui ya umaskini.  Kutokana na athari za umaskini, wazazi walihiari au kulazimika kuwapeleka watoto wao kufanya uzinzi.

iii. Yanakuza maudhui ya elimu.  Wasichana waliokuwa wametoroka shule ilhali wazazi wao walikuwa na uwezo walirejeshwa shuleni.

iv. Yanaonyesha uongozi mbaya.  Mtemi Lesulia na Sagilu walijua yaliyokuwa yakiendelea ila hawakushughulika.

v. Yanamulika ufisadi katika taasisi za serikali.  Sihaba anapokamatwa anaachiliwa siku iyo hiyo.

vi. Yanatumiwa kukuza vyombo vya dola.  Lonare na Mashauri wanamtumia jasusi ili kuchunguza mienendo ya Sihaba kwa siku mbili hivi.

vii. Yanajenga sifa za sihaba kama katili.  Anatumikisha wasichana    wadogo katika biashara ya ukahaba.

viii. Yanajenga dhamira ya mwandishi kwa kuonyesha athari za kujihusisha katika masuala yanayoenda kinyume na sheria.

ix. Yanaonyesha uozo wa maadili kutokana na wasichana wanauza miili yao.

 

 

 

 

MANDHARI KATIKA UGA WA KITAIFA

i. Yanaakisi hali halisi ya uchumi wa nchi ulivyo sasa.  Katika hotuba yake Lonare anasema kuwa jukumu kubwa lililo mbele yao ni kuukomoa Uchumi wa nchi unaozidi kudorora.

ii. Yanajenga maudhui ya ufisadi. Uchumi umekuwa ukifisidiwa na walafi wasiojali maisha ya wengi.  Wawekezaji na walafi     wasiojali maisha ya wengi.  Wawekezaji  wamehamia nchi jirani kutokana na ufisadi.

iii. Yanajenga maudhui ya tamaa na ubinafsi.  Wezi na walaghai wamekuwa wakichukua kibubusa raslimali za nchi kujinufaisha.

iv. Yanadhihirisha ukatili wa serikali ya awali.  Bidhaa muhimu zinafichwa na kuuzwa kwa bei ya juu. Hii insababisha mfumko wa bei.

v. Yanajenga maudhui ya umaskini. Kutokana na mfumko wa bei wananchi wanazidi huhasirika na kufukarika.

vi. Yanaonyesha jinisi ubadhirifu wa mali ya umma ulivyokuwa ukiendeleza katika serikali ya awali.  Kulikuwa na urudufu mwingi wa majukumu katika idara za serikali.

vii. Yanaakisi hali ya ukosefu wa kazi uliopo sasa hivi.  Lonare anasema kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wameuchimbia kaburi, kuuzika na kuusahau.

viii. Yanajenga maudhui ya nafasi ya vijana.  Vijana watahusishwa katika maendeleo ya nchi kinyume na ilivyokuwa awali walipopotosha wenzao na kuumbua uchumi.

ix. Yanajenga maudhui ya usawa wa kijinsia.  Serikali ya Lonare itazingatia usawa wa majukumu ya umma miongoni mwa wanawake na wanaume.

x. Yanaonyesha ulaghai wa wanasiasa.  Lonare anawaonya dhidi ya kuamini lugha ya wanasiasa kwani mara nyingi lugha hii hupindua usemi.  Huweza kupindua ukweli ukawa uongo na uongo ukawa ukweli.

xi. Yanajenga ploti kwa kuonyesha athari na usuli wa uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia. Huu ndio unafanya   wawekezaji wanahamia nchi jirani.

xii. Yanakashifu tabia za ukabila. Lonare anasema kuwa ukabila ni sumu ya nyoka. Huangamiza maendeleo ya nchi hata kama imestawi kiasi gani.

xiii. Yanajenga mtindo wa riwaya kupitia hutuba ya Lonare inayobadilisha mtindo wa usimulizi uliotumika.

xiv. Kupitia mandhari haya ploti inajengwa kwa kuonyesha hatima ya mgogoro wa uongozi baina ya Lonare na Mtemi Lesulia.  Lonare anachukua hatamu za uongozi na kutoa hutuba yake ya ushindi katika uga huu.

 

MANDHARI YA NYUMBANI KWA MRIMA

a) Kutowajibika – Mrima hawajibikii malezi ya wanawe jukumu hili analiachia mkewe.

b) Nafasi ya mwanamke – mwanamke ni mlezi mwema, mwenye mapenzi na mwabikaji.

c) Changamoto za ndoa – Mrima anamsaliti Mangwasha katika ndoa yao, anatelekeza familia

Yao na kuanza kufanya mambo yake ya ubinafsi na hatimaye kutorokea ulevini.

d) Yanajenga ploti – kupatikana kwa Mrima.

e) Yanajenga ukatili – Lonare anatendewa ukatili  visu hadi alipopatikana baadaye nyumbani mwa Mrima.

f) Ndoa – Mrima na Mangwasha ni wanandoa.

g) Mapenzi – Mangwasha anampenda mrima kwa dhati, anapenda kumfuata ponda mali na kumrudisha nyumbani.

h) Malezi – Mangwasha anawalea wanawe vyema licha ya kuachiwa jukumu na mumewe mtoro.

i) Uwajibikaji – Mangwasha anawajibika kuwalea wanawe hata baada ya kutelekezwa na Mrima.

j) Usaliti – Mrima anamsaliti Mangwasha kwa kugeukia pombe na kutomsaidia katika malezi.

 

MANDHARI YA OFISINI MWA CHIFU MSHABAHA

i. Yanaonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii kama kiumbe wa kuchaguliwa mume. Chifu Mshabaha anaudhika kuwa Mangwasha alikataa uhusiano-aliopendekeza chifu-  na Sagilu aliye na mali. (uk 19)

ii. Yanamsawiri Mangwasha kama mwenye msimamo dhabiti.  Mangwasha anashikilia msimao wake wa kuolewa na Mrima hata anaposhawishiwa na Chifu Mshabaha.

iii. Yanamsawiri Chifu Mshabaha kama mpyaro.  Anasema kuwa Waketwa in watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba.

iv. Yanadhihirisha ukatili wa Chifu Mshabaha.  Anamfukuza Mangwasha ofisini mwake. “Toka mbele yangu. Kwenda!” (uk 20)

v. Yanamchora Chifu Mangwasha kama mwenye dharau.  Anapomwita Mangwasha ofisini mwake anamdharau na mumewe kuwa hawakuwa na uweo hata wa kenda fungate ila walihitaji wasamaria kama yeye ili wawatoe kwenye shimo.

vi. Yanamsawiri Mangwasha kama mwenye heshima. Hata ingawa maneno ya Chifu Mangwasha yanamkera anaamua kunyamaza.

vii. Yanajenga maudhui ya Ukatili. Lonare anapomtembelea Mangwasha anamfahamisha kuhusu ukatili wa Mtemi Lesulia anayetaka wenyeji wa Matango wahame    eneo lile waende Ndengoni (uk 54)

viii. Yanajenga Ploti kupitia mkutano tunaoambiwa uliohusu machifu wote wa nchi ya Matuo na pia vijana walioandamana na chifu ofisini mwake. Hawa baadaye ndio wanakuja kuchoma makao ya wenyeji wa Matango.

ix. Yanaonyesha umuhimu wa vyombo vya habari katika kufichua maovu. Lonare anamwambia Mangwasha kuwa watatumia vyombo vya habari ili taarifa zifike mbali na kwa haraka kuhusu tisho la kuvamiwa kwa makao yao. (uk 56)

x. Yanamsawiri Mangwasha kama mshauri mwema. Anamshauri Lonare dhidi ya kuwa na kiburi,”Kumbuka kijapo kiburi ndipo ijapo aibu ndugu” (uk  56)

xi. Yanajenga ploti kwa kuonyesha hatima ya mgogoro baina ya Mshabaha na Mangwasha pale anapomfuta kazi.

 

MANDHARI YA MAHAKAMANI

i. Yanakuza maudhui ya dini. Waketwa wanapomwona Mwamba na jalada moja pekee wanainamisha vichwa na kumwomba Mungu.

ii. Yanajenga maudhui ya chuki. Waketwa wanapomwona Sagilu na Mafamba wakiingia mahakamani wanapiga vidoko na kujikohoza.

iii. Yanaendeleza maudhui ya unafiki.  Maelezo ya Mafamba kuwa wenyeji wa Matango walikuwa wamemiliki ardhi kwa vyeti ghushi inadhihirisha unafiki kwani walicho nacho wao ni halali.

iv. Ynaonyesha uadilifu wa jaji. Anaamua kesi kwa pupitia ushahidi ulipo ila si kwa ushawishi wa kina Sagilu

v. Yanaendeleza kutamauka.  Nyuso za Waketwa zilitangaza wazi ukosefu wa matumaini.  Walisubiri tu kesi iamuliwe wakatafute mahali pa kwenda.

vi. Ynajenga maudhui ya utetezi wa haki. Wenyeji wa Matango wanapeleka kesi mahakamani kutetea haki ya kumiliki ardhi wanayonyanga’anywa.

vii. Yanajenga ploti kupitia mgogoro uliopo baina ya wenyeji wa Matango na serikali ya Mtemi Lesulia kuhusu ardhi.

viii. Yanajenga ploti kutokana na hatima ya mgogoro baina ya Sagilu na wenyeji wa Matango kupitia uamuzi wa hakimu unaowahalalisha umiliki ardhi yao.

 

 

 

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Nguu za Jadi - Dhamira ya mwandishi

Nguu za Jadi - Sifa na umuhimu wa wahusika