Nguu za Jadi - Sifa na umuhimu wa wahusika

 SIFA NA UMUHIMU WA WAHUSIKA.

1. MANGWASHA

Huyu ndiye mhusika mkuu katika riwaya. Ni mkewe Mrima na mhazili wa Chifu Mshabaha.

Hulka za Mangwasha:

Mvumilivu

Mangwasha anavumilia matatizo mengi ndani ya ndoa yake yanayotokana na ulevi wa mumewe. Hata baada ya kukimbiwa na Mrima, anavumilia mateso mengi ya ukosefu wa pesa za kuwatunza wanawe, kukiwemo pia kejeli za Sagilu.

Mzalendo

Mangwasha anaonyesha uzalendo pale anapotamani kukutana na viongozi wa Matuo ili amani iweze kudumishwa nchini. Anajali sana mustakabali wa nchi ya Matuo hasa pale anapowaona watoto na vijana wakiteseka bila matunzo mema ya wazazi wao au hata ajira.

Mwenye matumaini

Haonekani kufa moyo bali anaonyesha matumaini pale Chifu Mshabaha anapomdharau na kumdhalilisha akiwa kazini. Anaonyesha matumaini pale anapohangaika kutunza wanawe dhidi ya mateso aliyokuwa akipitia alipokimbiwa na Mrima. Anapochomewa nyumba yake pamoja na wenyeji wa Matango havunjiki moyo bali anakuwa na tumaini.

Jasiri

Mangwasha anaonyesha ujasiri pale anapojitahidi kwa jino na ukucha kuiokoa ndoa yake kutoka kwa Sagilu aliyekuwa akiisambaratisha.

Kule kumsaka mumewe kwenye mabanda ya uuzaji wa pombe mbali na kukabiliana na walevi ni ishara ya ujasiri (uk. 34-36)

Mchapa kazi

Mangwasha ni mchapa kazi kutokana na bidii yake kazini. Alifanya kazi zote alizopewa na chifu bila manung'uniko na kufanya hata zile zilizopaswa kufanywa na topasi. Tunaambiwa alikuwa wa kwanza kufika kazini lakini wa mwisho kuondoka (uk. 14).

Mwenye upendo

Anampenda mumewe licha ya kwamba awali huyu alimtupa na watoto. Anaipenda jamaa na jamii yake kutokana na juhudi zake katika kuitunza jamaa yake na kushughulikia maslahi ya Waketwa wenzake. Anaonyesha upendo kwa watoto na vijana wa mitaani pale anapozungumza nao na kuwapa ushauri.

Umuhimu wa Mangwasha

a) Ni kielelezo cha upiganiaji wa haki kwa wanaoteswa na mifumo dhalimu ya kiutawala.

b) Ni kielelezo cha utokomezaji wa ukabila katika jamii.

c) Ametumiwa kuonyesha kwamba desturi na mila potovu katika jamii hazina nafasi katika jamii ya leo na kwamba zinapaswa kutokomezwa.

d) Ametumiwa kupiga vita ufisadi na maovu mengine yanayofanywa na viongozi.

e) Ametumiwa kuonyesha kwamba mwanamke anahitaji kushirikishwa katika sekta zote za umma licha ya kwamba ni mwanamke, na anahitaji kuheshimiwa.

f) Ametumiwa kutoa tahadhari kwa jamii kumjali mtoto wa kiume kwani hashughulikiwi ipasavyo.

 

LONARE

Lonare ni kiongozi wa jamii ya Waketwa na mpinzani wa Mtemi Lesulia.

Mtetezi wa haki kwa wote

Lonare anapigania haki za wananchi wote wa Matuo. Habagui watu kwa misingi ya ukabila au jinsia yao bali anasimamia haki na usawa wa wananchi wote. Anamhamasisha Mangwasha kupigania haki za vijana bila ubaguzi na anasomesha watoto wake wote bila ubaguzi wa kijinsia.

Mvumilivu

Lonare anavumilia vitisho juu ya maisha yake vinavyoendelezwa na Mtemi Lesulia ikibainika kwamba anatishiwa uhai wake zaidi ya mara moja. Anavumilia biashara yake ya usafiri wa magari ya umma inapoathiriwa na vitendo dhalimu vya wafuasi wa mtemi hasa pale magari yake yanapokamatwa kwa makosa madogomadogo na madereva wake kupigwa faini (uk. 50).

 

Mkombozi/mwanamapinduzi

Anaingia katika kampeni za kisiasa bila kujali vitisho vya mtemi ili kuikomboa nchi yake, azma nayotimiza na kuwa mtemi wa Matuo.

Akishirikiana na Mangwasha na wengine, anamkomboa Mrima kutoka katika maisha ya anasa na ulevi na kurudia familia yake.

Jasiri

Kuwania kiti cha mtemi wa Matuo licha ya vitisho na masumbufu aliyopitia, ni ishara ya ujasiri. Kupitia kwa ujasiri wake, anahiari kupitia mateso ya kutekwa nyara na kuumizwa lakini hakuvunjika moyo hadi anaposhinda uchaguzi na kuwa mtemi wa Matuo. Magari yake ya usafiri yanapokamatwa kwa visingizio visivyokuwa na maana hadi madereva wake kutozwa faini zisizoeleweka, hakuvunjika moyo bali aliendelea na biashara hiyo.

Mzalendo

Lonare anaipenda nchi yake kiasi cha kuhatarisha maisha yake ili aikomboe kutoka katika utawala dhalimu wa Mtemi Lesulia. Anawathamini raia Wote wa Matuo bila ubaguzi wa kikabila kwani tunaambiwa aliweza hata kuajiri watu kutoka katika jamii ya Wakule. Hotuba anayotoa baada ya ushindi wake ni kielelezo cha uzalendo; anawataja raia wote wa Matuo kuwa ndugu zake na kuwahimiza kuungana 'ili kujenga nchi yao. Kauli Zinazoashiria uzalendo wake ni kama pale anaposema kwamba ukabila ni sumu ya nyoka na kwamba huweza kuangamiza maendeleo ya nchi.

Mshauri mwema

Ushauri wa Lonare unaonekana pale anapomshauri Mangwasha awe na subira katika kutatua matatizo yaliyowakabili. Tunamwona pia akimshauri Mrima kwa kutumia mafumbo ili aweze kubaini maana ya ndani. Kwa mfano, anamwambia kwamba ajifunze kutokana na makosa yake mwenyewe (uk. 101), na kwamba kamwe hawezi kusalimiana na mtu aliyekunja ngumi (uk. 114). Pia anamshauri Ngoswe kuacha kufanya biashara haramu na kufunga majumba ya ufasiki anayomiliki kama anaipenda nchi yake (uk. 171).

MTEMI LESULIA

Huyu ni kiongozi wa nchi ya Matuo na mumewe Nanzia. Anajitokeza pia kama rafiki shadidi wa Sagilu.

Sifa za Mtemi Lesulia:

Mwenye tamaa na ubinafsi

Tamaa yake inagawika kuwili; tamaa ya uongozi na tamaa ya mali na utajiri.

Ni kielelezo cha uongozi mbaya kutokana na jinsi anavyojilimbikizia mali bila kujali raia wake. Ana tamaa ya kusalia mamlakani; tunamwona anafanya juhudi zote hata kujaribu kuua wapinzani wake ili asalie mamlakani. Tamaa yake inafanya uchumi wa nchi kuzorota kutokana na sera mbaya za uongozi; akiwa na wenzake, anahujumu pato la nchi kutokana na ubinafsi wake. Tamaa ya mali inamfanya kujaribu kuwapoka wenyeji wa Matango ardhi yao.

Fisadi

Ufisadi unamfanya Mtemi Lesulia kuajiri watu wasiokuwa na ujuzi au utaalamu katika sekta za umma huku akiacha wale wenye ujuzi (uk. 44). serikali yake inaajiri watu kwa kujuana huku ajira zikitolewa kibubusa.

Ufisadi katika serikali yake unafanya mashirika na taasisi za serikali kumilikiwa na mitandao ya wezi huku akisaidia katika kuipoka nchi hadhi yake. Katika serikali yake "Ufisadi uliikithiri na maadili yakawapa mkono wa buriani" (uk. 45).

Ni katili.

Mtemi Lesulia anadhihirisha ukatili pale ambapo anaungana na wengine kumpangia Lonare njama ya kuharibu biashara yake. Anapompangia njama ya kumuua au hata kufanya atekwe nyara wakati uchaguzi mkuu unapokaribia ni ishara ya ukatili wake, Hakujali pale watoto na vijana nchini mwake walivyokuwa wakiteseka kutokana na mifumo mibaya ya uongozi wake.

Mwenye dharau

Anawaita wenyeji wa Matango panya baada ya kuchomewa nyumba zao na kurejea tena katika makao yao (uk.78). Anaonyesha dharau kwa mwanawe mbele ya rafiki zake anaposema, "Toto hili! Hata sijui lilitoka wapi." (uk.129).

Mwenye ukabila

Utawala wake unatawaliwa na ukabila mwingi. Anawanyanyasa Waketwa na kuwathamini Wakule ambao ni jamii yake. Hili linabainika anapokosa kuwaajiri vijana Waketwa waliohitimu. Hawa anaajiriwa kufanya kazi za kijungujiko kama vile wafanyakazi katika mashamba ya matajiri.

MsalitiAnaisaliti nchi na watu wake kutokana na uongozi mbaya usiojali maslahi ya wanyonge. Anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kuwatenga katika ajira licha ya kwamba wao pia anastahili kuwajibikiwa kama Wakule. Anamsaliti mwanasheria Mafamba aliyefanya kilajuhudi za kumfichia maovu ya serikali yake kwa kumnyang'anya cheti cha uanasheria na kumtimua kutoka katika mji wa Taria. Kitendo cha kumnyang'anya hakimu cheti chake cha uanasheria na kumfuta kazi ni usaliti kwani hakimu alikuwa akitekeleza majukumu ya utetezi wa haki nchini mwake.

SAGILUSagilu ni rafiki mkubwa wa Mtemi Lesulia na mzazi wa Mashauri na Ngoswe.

Mwenye ukabila

Anaonyesha ukabila pale ambapo anahiari kushirikiana na wengine kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba zao akijua kwamba jamii ya Waketwa iliyokuwa na idadi kubwa iliishi humo.

Ukabila unamfanya kushirikiana na Mtemi Lesulia ili Lonare ambaye ni Mketwa asichukue kiti cha mtemi wa Matuo. Kauli za Sagilu pia zinaonyesha ana ukabila hasa anaposema, "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka" akimaanisha Waketwa

FisadiSagilu anajiingiza katika vitendo vya ufisadi hasa kutokana na urafiki wake wa karibu na Mtemi Lesulia. Tunamwona akishirikiana na mwanawe Mashauri kufisidi nchi kwa kuuza vipusa na meno ya ndovu (uk. 127). Anatowesha bidhaa na kuziuza kwa faida.' "...alizuia meli nzima baharini isitie nanga bandarini na kupakua ngano hadi alipofaulu kuuza kwa bei ya juu ngano yote nchini." (uk. 17).

Mwenye ukabilaAkiwa na Mtemi Lesulia, walimiliki viwanda kadha ambapo waliwaajiri Wakule pekee (uk. 7). Anafanya kila njia Lonare na Mwamba wasiweze kushinda katika uchaguzi wa kisiasa kutokana na hisia za kikabila. Hii ni kwa sababu wao si Wakule kama yeye. Anamdhihaki Mangwasha kwa kumwambia, "Nyie Waketwa ni watu wa ajabu sana. Mwanzo Mwamba ni nani kwangu? Yule ni sawa na kidagaa tu." (uk. 103).

Tunaona akionyesha hisia za kikabila baada ya wao kushindwa katika uchaguzi mkuu pale anapowaza juu ya Mangwasha na kusema, "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka. Mtawezaje kuruka ilhalimnaishi mkifikiria kwamba kuruka ni ugonjwa?" (uk. 176).

Mwenye wivuSagilu hataki wengine wampiku katika biashara kwani anataka kila biashara anayofanya pasiwe na wa kushindana naye. Wale wanaomshinda, anatumia hila na werevu hadi kuwashinda kibiashara (uk. 16). Wivu unamfanya kumkabili Mrima alipokuwa akimposa Mangwasha kwani hata yeye alimtaka. Anapomwambia, "Kijana, fahamu kwamba nahodha haogopi mawimbi." (uk. 19) ni ishara ya husuda aliyo nayo, Anamkabili Mangwasha huku akimtazama kwa jicho la husuda pale anapofahamikiwa kwamba huenda akashindwa na Mwamba katika uchaguzi (uk. 103).

MsalitiAnawasaliti wenyeji wa Matango kwa kushiriki katika kuwachomea makazi yao huku akijua kwamba alitaka kuwa mgombea kiti wa eneo hili kupitia kwa chama cha mtemi. Anamsaliti Mrima huku akijifanya ni rafiki yake pale anapompa pesa za kumlewesha na kujitenga na familia yake. Anaisaliti jamii nzima ya Matuo kwa kuwauzia maziwa ya watoto yenye sumu bila kujali ingewadhuru watoto hao, mbali na kuwauzia bidhaa ghushi bila kujali afya yao. Mpenda anasa Anajivinjari na wanawake kama vile Sihaba bila kujali kuwa ana mke.

CHIFU MSHABAHA

Chifu Mshabaha ni mwajiriwa katika serikali ya Mtemi Lesulia.

Sifa za Chifu Mshabaha:

Mwenye ukabila

Madhila anayopitia Mangwasha kazini chini ya uongozi wake yanatokana na ukabila. Chifu anatoka katika jamii ya Wakule ilhali Mangwasha ni Mketwa. Chifu anamwambia Mangwasha kuwa, "Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba...mnabaki nyuma kama makoti." (uk. 20) kuonyesha chuki yake kwa jamii ya Waketwa.

Fisadi

Anapokea hongo baada ya kujishughulisha katika harakati za kuwapokonya wenyeji wa Matango ardhi yao ili wakabidhiwe Nanzia na Mbwashu. Anamkabidhi Mrima pesa alizopokea kutoka kwa Sagilu kama hongo ili kumshawishi amfanyie mtemi kampeni ilhali akijua yeye alikuwa mfuasi wa Lonare (uk. 105). Anapomchukua msichana kutoka katika jamii yake ili kufanya kazi katika afisi yake badala ya Mangwasha ni kielelezo cha ufisadi. Hakukuwa na makosa yoyote ya kumfuta Mangwasha kazi ila alitaka kumwondoa pale ili asiweze kubaini maovu aliyokuwa akifanya kwa niaba ya serikali ya Mtemi Lesulia.

Katili

Ukatili wake unaonekana pale anaposhirikiana na Sagilu, Sihaba na wengineo kuwapoka watu wa Matango ardhi yao. Anamtendea Mangwasha uovu pale anapomfukuza kazi na kumleta msichana kumfanyia kazi badala yake. Anamfedhehesha Mangwasha na kumwonyesha dharau licha ya kwamba huyu anamfanyia kazi kwa utiifu na heshima.

Msaliti

Anaisaliti jamii ya Waketwa na wote waishio Matango kwa kushiriki katika njama ya kuwaondoa kutoka katika makao yao; tunaona mipango ya kuwaondoa ikitekelezwa ndani ya afisi yake. Anamsaliti Mangwasha kwa vile alipokea bahasha ya pesa kutoka kwa Sagilu na kumpelekea.

Mwenye dharau

Anamwonyesha Mangwasha dharau akiwa kazini kwa kutumia lugha isiyo na heshima. Kwa mfano, anamwambia Mangwasha Waketwa hawana akili hata ya kuchagua wachumba (uk.20). Anaonyesha dharau pia pale anapomwambia Mangwasha hawana pesa hata za kuwapeleka katika fungate yao baada ya arusi, au kumdhihaki kwa kusema, "Hata kama hamtaenda kokote, mtakaa nyumbani mkipanga kuwa na jeshi la watoto..." (uk. 23). Baada ya kuwatembelea watu waliochomewa nyumba zao pale kanisani walipojisitiri, alitamka maneno ya dharau yaliyowasha moto wa ghadhabu (uk. 70).

MRIMA

Mrima ni mfanyakazi wa serikali, mfanyabiashara na mumewe Mangwasha.

Sifa za Mrima:

Mwenye tamaa na ubinafsi

Ana tamaa ya pesa hasa pale anapokubali kuitelekeza jamaa yake kwa kufuata pesa za Sagilu ili kujistarehesha. Anathibitisha hili kwa kusema, "Mhn, ati familia? Kwani mimi mjinga niache mapesa haya yote yanipite bila kuyafaidi." (uk. 37). Tamaa ya pesa na ubinafsi inamfanya kukaidi masharti ya ndoa na kutomjali mkewe na watoto. Anasema, "Siku hizi kila mtu anazisaka chapaa, haijalishi ni kwa njia gani..." (uk. 107).

Mpenda anasa na ulevi

Anapotelea Ponda Mali na Majaani, mahali palipokuwa na walevi wa kila aina ili kujihusisha na ulevi. nakuwa mlevi kupindukia kiasi cha kutoweza kuitunza familia yake. Anafanya usuhuba na wanawake nje ya ndoa kutokana na barua ya mahaba anayoipata Mangwasha (uk. 77) na ambayo iliandikwa na mwanamke.

Mhafidhina

Anatoa kauli zinazoonyesha kwamba ingawa ni kijana wa kisasa, bado ameshikilia mawazo na itikadi za utamaduni wake. Kwa mfano, anasema, "Tangu lini mke amuulize mumewe kule aendako au atokako?" (uk. 40). Baada ya kutibiwa katika hospitali kutokana na uraibu wa pornbe, anakataa kwenda kwake. Tunaona akiuliza swali, "Hamwoni kwamba mila hairuhusu mie nikatunzwe na mke kama mgonjwa?" (uk. 100).  

SIHABA

Sihaba ni rafiki ya Sagilu anayemiliki makao ya Red Beads Lodgings. 

Sifa za Sihaba:

Fisadi

Anatumiwa na Sagilu kuendeleza vitendo vya ufisadi. Anatumiwa kuangamiza washindani wa Sagilu kibiashara. Anatumiwa katika uchomaji wa nyumba za wenyeji wa Matango kwa usambaza vijikaratasi kuwaambia wahame. Anapokamatwa na kutupwa korokoroni kutokana na kusambaza vijikaratasi au kuwatumia watoto katika biashara ya ukahaba, tunaambiwa hakukaa humo bali anatumia njia za kifisadi na kutoka bila kufunguliwa mashtaka.

Katili

Anashirikiana na Sagilu kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba. Ukatili wake unaonekana pale anapojifanya kuwapelekea Mrima na Mangwasha zawadi ya arusi ilhali kilikuwa kifurushi cha kilipuzi. Kule kuwachukua wasichana wadogo na kuwaingiza katika biashara ya ukahaba bila kujali maisha yao ya baadaye ni ishara ya ukatili.

Mnafiki

Anakwenda kuwapa zawadi Mrima na Mangwasha siku ya arusi yao lakini haikuwa zawadi bali kilipuzi cha kuwaangamiza. Anajifanya kuwa na urafiki na wakuu wa serikali huku akijipendekeza kwao ilhali lengo lake ni kujinufaisha kiuchumi na kuishi maisha ya anasa.  

Mnyanyasaji wa haki za watoto

Umuhimu wa Sihaba

1. Ametumiwa kuonyesha jinsi wanawake wanavyoweza kutumiwa na wanaume kama vyombo vya kuendeleza maovu katika jamii.

2. Ametumiwa kuendeleza madhara ya ukabila katika jamii.

3. Ni kielelezo cha wale wanaovurujua haki za watoto kwa manufaa yao binafsi.  

MASHAURI

Mashauri ni mwanawe Sagilu na rafiki ya Lombo na Ngoswe.

Sifa za Mashauri

Fisadi

Tunaona Mashauri akiajiriwa na Mtemi Lesulia kama mtaalamu mkuu wa usanifu majengo mjini Taria. Pale mwanzo Mashauri anaonekana akishirikiana na baba yake kufisidi vipusa na meno ya ndovu. Anauza maliasili za nchi ng'ambo hadi anaathiri utalii nchini, huku akitumia cheo chake kuzima mashtaka yaliyofikishwa kortini (uk. 127). Kutokana na cheo chake kama msimamizi wa ujenzi wa majengo, ana uwezo pia wa kuamuru kubomolewa kwa majengo yasiyojengwa kihalali au yasiyokuwa salama (uk. 117). Nafasi hii inamfanya kuchukiwa na watu kutokana na ubomoaji wa majengo Taria.

Katili

Ukatili wake unabainika pale alipoamuru majengo ya watu kubomolewa kiholela kwa mpigo wa kalamu yake (uk. 127). Anashirikiana na babake kufuja rasilimali za nchi na kusafirisha ng'ambo bila kujali hatima ya uchumi wa nchi yake au hata wananchi waliotegemea rasilimali hizo. Anadidimiza utalii nchini bila kujali matokeo kwa nchi yake.

Msamehevu

Licha ya kwamba Sagilu anamtendea maovu kumwendea kinyume, anamsamehe na hata kumtafutia matibabu ya akili.

Mvumilivu

Anamvumilia Sagilu hata baada ya kumkosea, akamchukua kutoka barabarani na kumpeleka kupata matibabu ili kuficha aibu. Anavumilia kauli za kuvunja moyo kutoka kwa Sauni na wengine wasiomwamini, akajiunga na Chama cha Ushirika cha Lonare ili kumfanyia kampeni.

Fisadi

Anajiingiza katika biashara haramu ya mihadarati na anatumia mitandao ya wahuni kufanya biashara hiyo ambayo ni kinyume na sheria za nchi. Pia anafisidi mali ya babake kutokana na usimamizi wa mashamba na majumba yake. Pesa alizofuja pia anawekeza katika majumba ya starehe (uk. 123).

MleviAnaonekana kuwa mlevi hasa pale katika hoteli ya Saturn tunapoambiwa kwamba alikuwa amepiga maji kupindukia" alipomkabili Sagilu na kumwaibisha mbele ya watu (uk. 134).  

 

Mwenye msimamo thabiti

Mtemi Lesulia anapowashawishi rafiki zake waende kufanya fujo wakati wa uchaguzi, Ngoswe anakataa katakata ushauri wa mzazi wake na kujiondoa kutoka katika mazungumzo hayo (uk. 129). Anaamua kumwambia Mashauri kuhusu uhusiano wa Cheiya na babake, liwe liwalo. Hakujali kuvunja uhusiano wa Mashauri na babake bali alitaka ukweli ujulikane (uk.120-125).  

 

Comments

Popular posts from this blog

Nguu za Jadi - Madhari katika riwaya

Nguu za Jadi - Dhamira ya mwandishi