Nguu za Jadi - Dhamira ya mwandishi

                                

                                                Dhamira ya mwandishi

Dhamira ni shabaha,nia, kusudi, au lengo kuu la kazi ya fasihi. Aidha inaweza kuwa ni shinikizo kuu liliopelekea utunzi au uwasilishaji wa kazi za kisanaa fasihi ikiwemo.

Katika riwaya ya Nguu za Jadi, mwandishi anamulika masuala yafuatayo:

a) Anakemea ukabila uliosakini katika jamii na unaodumaza maendeleo ya nchi.

b) Anatuonyesha jinsi ufisadi unavyoweza kubomoa asasi za kijamii na kufukarisha wananchi kiasi cha kutoweza kujiendeleza kimaisha.

c) Anatuonyesha jinsi ufisadi unavyoweza kusambaratisha uchumi wa nchi hasa pale unapochangiwa na uongozi mbaya kama vile ilivyotukia katika riwaya ya Nguu za Jadi.

 

MAUDHUI KATIKA RIWAYA YA NGUU ZA JADI

Ukabila/Unasaba

Ukabila ni hali ya kupendelea mtu, watu au Jamii fulani kutokana na misingi ya jamii/kabila alimotoka. Upendeleo huu huweza kuhusisha mambo mengi kama vile ajira, elimu, makazi, vyeo, na kadhalika. Katika riwaya hii, ukabila unadhihirika ifuatavyo:

a) Wakule ni jamii inayoonyesha ukabila; wao ndio wengi serikalini (uk. 43) kutokana na hali kwamba Mtemi Lesulia ambaye ndiye kiongozi wa nchi ya Matuo anatoka katika jamii hii. Wakule wengi hasa walio matajiri wanajitenga na kuishi katika mtaa wa Majuu ambao ni mtaa linamoishi tabaka tawala.

b) Vijana wa Waketwa wanatengwa na kukosa kazi kwa kuwa wanaopeana hizi kazi ni wa jamii ya Wakule; viongozi wa jamii hi wanahakikisha kuwa Waketwa wanakosa kazi.

c) Mangwasha anadhulumiwa na Chifu Mshabaha kwa misingi ya kikabila. Anawatukana Waketwa na kuwaita watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba.

d) Wanawake Waketwa walioolewa na wanaume Wakule wanaobahatika kupata ajira serikalini wanapoguduliwa wanfutwa kazi kwa visababu duni.[ Uk 45]

e) Sagilu anawadharau Waketwa na kuwaona kama watu wasioweza kuongoza, “Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka…mnaishi mkifikiria kuruka ni ugonjwa?”

f) Makao ya Waketwa yalichomwa huko Matango kwa sababu a kikabila; walihitaika kufurushwa ili wasimpigie mmoja wao kura. Aidha sehemu hiyo ilikuwa imepewa wawekezaji wa jamii ya Wakule.

g) Mtemi Lesulia amawadharau Waketwa akirejelea ukabila, anawaita panya alipokuwa akizungumza na Sagilu kuhusiana na ardhi ya Matango.

h) Chifu Mshabaha anamfuta kazi Mangwasha na kumwajiri mhazili wa jamii ya Wakule, anasingizia kuwa akina Mangwasha walikuwa wakipiga siasa na kupinga serikali iliyomwajiri

Utabaka

Utabaka ni hali inayosababisha jamii kujibagua katika makundi tofauti kutegemea uwezo wao wa kiuchumi. Makundi haya huwa matatu, la kwanza ni tabaka  la chini. Hawa ni wale wasioweza kugharamia mahitaji ya kimsingi kama vile vyakula, makazi mazuri au hata mavazi. Watoto wao husoma kwa shida au hata hushindwa kuwasoma kabisa.Pia hujulikana kama maskini,walala-hoi, akina yahe, makabwela, akina pangu pakavu. Pia kuna tabaka la kati linalojumuisha wale walio na uwezo wa kadiri, hawa ni wafanya kazi wanaosumbuka kwa kiasi kulimbua riziki japo hawasumbukii mahitaji ya kimsingi.  Tabaka la mwisho ni lile la juu, tabaka hili ni la wale walio katika utawala au biashara kubwa kubwa, wanaweza kugharamia chochote na hata kufanya lolote pia hujulikana kama matajiri, walala-heri, wamwinyi, makabila au wakwasi. Matabaka yanayobainika sana ni  mawili; matajiri na maskini au wenye mali na vyeo na wasio navyo.

a) Utabaka unaonekana katika jumuiya inayozungumziwa (uk. 7). Nchi ya Matuo inazingatia utabaka. Kuna tabaka la juu linalohusisha wakwasi, matajiri na wakuu wa serikali ambao pia wamejitenga na kuishi katika mtaa wa kifahari uitwao Majuu (uk. 7 na uk. 51).

b) Wananchi wa kawaida wanaishi katika mitaa ya matabaka ya chini na yale ya kati kama vile Majengo, Matango na Majaani. Hawa wanahusisha wanaofanya kazi viwandani, mashambani, makarani, matarishi, matopasi au vibarua wanaofanya kazi za shokoa.

c) Tunaarifiwa nchi ya Matuo ilishikilia utabaka (uk. 45), "...matajiri wakawa wenye nchi na wananchi wengine  wakasalia kuwa wana wa nchi". Maudhui ya utabaka yanaonyesha kuwa tabaka la juu ndilo lililomiliki nyenzo za uzalishaji mali na ndilo lililohujumu dhamana na hawala za serikali. Tabaka hili linahusisha watu kama vile Mtemi Lesulia, Sagilu, Nanzia, Mbwashu, hata Ngoswe-mwanawe mtemi ambaye anaishi katika kasri la kifahari.

d) Maudhui ya utabaka pia yanabainika kupitia mhusika Mangwasha anaposhangaa kumwona Mbwashu akiwasili pale kanisani kwa gari aina ya Land Rover kumaanisha kwamba hadhi yake haimruhusu kutumia gari kama lile (uk. 68). Aidha, mke wa Mtemi Lesulia naye anawasili pale kwa gari aina ya Pick Up (uk. 71).

Uongozi/Utawala mbaya

Maudhui ya uongozi mbaya yamegawika kuwili; uongozi mbaya serikalini na katika familia.

a) Uongozi mbaya serikalini unaonekana kupitia kwa Mtemi Lesulia ambaye alitawala kwa mkono wa chuma na 'kauli alizotoa zilichukuliwa kama sheria za nchi' (uk. 7).

b) Mtemi anaonekana kuogopwa na raia wake na hili linabainika pale Mrima anapomkanya mkewe asijaribu kukutana na mtemi kumaanisha kwamba si mtu mzuri, na raia walimwogopa (uk. 8). Mtawala hapaswi kuogopwa na raia wake bali anapaswa kuheshimiwa kama vile raia walivyomheshimu Lonare.

c) Uongozi mbaya pia unaonekana kupitia kwa kiongozi huyu ambaye anashirikiana na makundi ya wahuni kuwanyanyasa raia wengine(Waketwa) kwa kuwachomea makazi yao. Hii ni ishara ya uongozi mbaya wa kutenga na kubagua raia kwa sababu ya ubinafsi unaotokana na siasa za ubaguzi na chuki.

d) Uongozi mbaya unaendelezwa pia na Chifu Mshabaha; kumnyanyasa Mangwasha kazini na kutojali kazi nyingi anazotekeleza katika afisi yake. Pia hakujali kuhujumu hata mambo yaliiyohusu familia yake na masuala ya kibinafsi kama uchumba au hata mahudhurio ya harusi iliyohusu mafanyi kazi wake wa karibu.

e) Mtemi Lesulia anaongoza kupitia marafiki wake wa karibu. Hawa ni kama vile Sagilu na wenzake ambao walitumwa kutekeleza majukumu maovu kama vile kuharibu mipango ya wapinzani wake ili aendelee kubaki katika uongozi.

f) Chifu Mshabaha anamnyanyasa Mangwasha katika mahali pa kazi. Alimpa kazi nyingi hata zile zisizoshahili. Pia alikuwa akimkemea na kumkaripia hata kwa sababu duni na zile ambazo hazikuhusiana na utendakazi bali ukabila.

Ufisadi

Ufisadi unahusu utumiaji mbaya wa mali ya shirika,chama au serikali, pia ni taabia ya ubadhirifu. Ufisadi umejitokeza kwa njia mbalimbali kupitia kwa baadhi ya wahusika na unachukua sehemu kubwa katika riwaya hii. Aidha, kuna ufisadi uaohusu maadili katika familia ambako mume au mke humwendea kinyume mwenzake na hili lipo kwa kiasi kikubwa katika riwaya ya Nguu za jadi.

a) Kutozingatia ujuzi, maarifa au taaluma ya mtu katika upeanaji wa ajira kunasababishwa na ufisadi. Serikali ya Mtemi Lesulia inawaajiri watu wasiokuwa na ujuzi wala maarifa huku walio na uwezo huo wakiachwa (uk. 44). Tunaambiwa ajira zinatolewa kibubusa na kwa kujuana hasa katika misingi ya ukabila. Hali hii inasababisha hujuma katika uajiri na kuzorotesha uchumi wa nchi.

 b) Ufisadi unasababisha ukiukaji wa maadili ya kifamilia kwani tunaona mauaji ya kifamilia yakikita mizizi. "Mume anamgeukia mke na kumchinja, naye mke akafanya vivyo hivyo." (uk 47).

c) Taasisi na mashirika ya serikali yanamilikiwa na mitandao ya wezi na hivyo kuipoka nchi hadhi yake (uk. 47). Rasilimali ya nchi inafujwa na watu walioshabikia wizi kama vile Ngoswe na akina Sagilu.

d) Polisi nao wanaendeleza ufisadi pale wanapowatoza madereva wa Lonare faini zisizoeleweka; pale Lonare anapohangaishwa na polisi kwa makosa madogomadogo; kupokonywa leseni, na kadhalika.

e) Vijana wanahongwa ili wafanye maovu ya kuwachomea wenyeji wa Matango makazi yao. Akina mama waliripoti kukutana na vijana wabebeba mageleni matupu yaliyonuka mafuta. Walionekana waiingia katika gari la Sihaba.

f) Sagilu anamhonga Mrima mara kwa mara,alimpa kitita cha pesa ili aingilie ulevi na kuitelekeza familia yake. Mara ya kwanza aliokolewa na mkewe na akina Lonare; baadaye alipewa shilingi elfu mia nane ili akubali kumfanyia amtemi Lesulia kampeni. Aliahidiwa kazi nzuri, na pesa zaidi juhudi zake zikionekana (uk 110).

g) Nanzia mkewe Lesulia alinyakua jumba refu lililomilikiwa na mlowezi mmoja aliyefurushwa nchini na kulibadilisha jina kuwa Skyline Mall. Huu ni ufisadi.

Utamaduni

Utamaduni ni ujumla wa maisha ya watu. Pia ni mila, desturi, asili, imani na itikadi za kundi la watu au jamii fulani. Aina mbili za maudhui ya utamaduni zinajitokeza katika riwaya hii.

Kuna utamaduni wa kiasili ambao unazingatia jadi na desturi za kiasili za jamii zinazozungumziwa.

Kwa ujumla wake, jumuiya ya Nguu za Jadi ni ile inayozingatia mfumo wa kuumeni. Huu ni mfumo unaompa mwanamume nguvu na mamlaka zaidi ya mwanamke. Mfumo huu unajulikana pia kama mfumo wa ubabedume au taasubi ya kiume ambao humweka mwanamume katika nafasi ya juu kijamii akilinganishwa na mwanamke.  

Ubabedume ni hali inaonyesha nafasi ya mwanaume katika jamii fulani na pia dhuluma wanazopitia wanajamii wengine kwa kuwa jinsia ya kiume ndio viongozi na wasemaji wa jamii, hivyo basi jinsia ya kike haina husemi katika jamii husika hata wakidhulumiwa pasipo kukosa. Mfumo huu pia unagawanya majukumu tofauti baina ya mwanamume na mwanamke kulingana na jinsia yao na kusisitiza kuwa kila jinsia ifanye kila jukumu bila kuingilia majukumu wa ile jinsia nyingine.Hali hii inadhihirika ifuatavyo katika riwaya:

a) Mangwasha hakutarajiwa kuongea na viongozi wa jamii yao kuhusiana na hali yao kwa sababu yeye ni mwanamke.( Uk 8)

b) Utamaduni ulishinikisha mwanamke kumheshimu mwanamume. Mbungulu anamwambia Mangwasha kuwa hafai kumfuata mumewe katika maeneo ya starehe kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na tamaduni alizofunzwa unyagoni. (Uk 32)

c) Mrima anaibua maudhui ya utamaduni anaposema kuwa yeye ni mwanamume na kuwa mkewe hangemzuia kuoa mwanamke mwingine. Anasisitiza kuwa jamii inaruhusu ndoa za mke zaidi ya mmoja. (Uk 41)

d) Mrima alipookolewa kutoka ulevini, alichelea kurudi nyumbani kwani angerudi kule bila kazi akatunzwe na mkewe. Aliona hilo kuwa kukiuka utamaduni wao. (Uk 100)

Kuna ule utamaduni unaokumbatia usasa. Utamaduni huu unaotokana na maisha ya kimji na athari zake. Athari hizi ndizo  ambazo zinachukua sehemu kubwa ya maudhui haya.

Hali hii inajitokeza kupitia hatua na ujasiri wa Mangwasha kwa vile anavyojizatiti kukiuka baadhi ya vikwazo vilivyowekwa na tamaduni kama vile kwenda kumtafuta mumewe katika maeneo ya ulevi, kuongea na viongozi kuhusiana na matatizo yanayohusu jamii yao, kuwa jasusi wa siri wa akina Lonare yote ambayo yalitoa mchango chanya katika ukombozi wa jamii yao.

Maisha ya anasa, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya

Ufasiki ni tabia ambayo hukiuka maadili ya kijamii. Tabia kama hii huhusishwa na uzinzi au uzinifu. Tunaonyeshwa jinsi Sagilu anavyoishi maisha ya anasa huku akifanya usuhuba na wanawake kama Sihaba nje ya ndoa. Anawanyang'anya wanaume wake zao hadi kuitwa mnyakuzi na dudumizi (uk. 18). Anamhangaisha Mangwasha kutaka kufanya usuhuba naye, hata kutaka kumhonga kwa kutumia pesa ili akubali (uk. 30, 60).

Ufuska wake unaonekana pia pale Mrima anaposema Sagilu alikuwa na masuria watoshao kijiji kizima (uk. 18). ufuska wa Sagilu unakia mipaka pale ambapo alijihusisha kimapenzi na mchumba wa mwanawe Mashauri Cheiya katika mkahawa wa Saturn. Kitendo ambacho kiliharibu uhusiano wake na Mashauri na hatimaye kugharimu nafasi yake ya uongozi.

Mrima anatumbukizwa katika anasa na kushiriki ulevi na Sagilu (Uk. 30, 37, 39, 42). Anashindwa hata kuitunza jamaa yake. Barua aliyoandikiwa Mrima na mwanamke fulani na  ambayo inapatikana ndani ya mkoba wa Mangwasha pamoja na yaliyomo katika barua hiyo ni ishara ya maisha ya uzinzi aliyoishi Mrima licha ya kuwa katika ndoa. (uk. 77).

 

Tamaa na ubinafsi

Tamaa ni hali ya kutaka sana kitu, matamanio ya kitu au jambo. Ni matamanio ya kitu au jambo; hamu shauku au ashiki. Tamaa kama hamu au utashi mkubwa wa kufaidi kitu huwa mbaya iwapo utafaidi mtu mmoja kutokana na ubinafsi wake au kundi la watu lenye maslahi yanayofanana na kumwacha mwingine na uhutaji aliokuwa nao.

Ubinafsi unahusu tabia ya mtu kujali maslahi yake mwenyewe na kupuuza ya wengine. Ubinafsi hubainika pale mhusika anapojipendelea yeye au kujifikiria yeye mwenyewe bila ya kuwajali wahusika wengine. Kuna wahusika kadha wanaoendeleza maudhui ya tamaa na ubinafsi hasa pale mwandishi anapotaja kuwa;

a)  Mtemi Lesulia, akiwa na wakwasi wenzake kama vile Sagilu na Mbwashu wanahujumu pato la nchi kutokana na tamaa ya kujilimbikizia mali. Wanapofanya hivi wanaishia kujifaidi wao wenyewe tu.

b) Sagilu anapohodhi bidhaa kama vile ngano ili kuiuza kwa bei ya juu akiwapuja wateja ni dhihirisho la tamaa. Pia Sagilu anauza maziwa yenye sumu akihatarisha maisha ya watoto (Uk 17)

c) Sagilu anawafanyiaa mizungu na kuwafiisi wale wlioshindana naye kibiashara. (Uk 16)

d) Sagilu ni kielelezo cha wahusika walioshindwa na ashiki za kimwili, kwa sababu ya ubinafsi wake anawanyemelea wasichana kama vile Mangwasha hadi alipoolewa na Mrima, alisemekana kuwabadilisha wanawake hata kuwachukua wake wa waume wengine. (Uk 18)

e) Sagilu anazini na Nanzia, mkewe mtemi Lesulia na kupata mvulana Ngoswe. Kilele cha tamaa zake ni kuzini na mchumba wa mwanawe aliyeitwa Cheiya.

f) Nanzia ana tamaaa ambayo ilimfanya kushiriki ngono na mhindi aliyekuwa mshirika wa kibiashara na Mtemi Lesulia. Katika uhusiano huu, alipata mvulana aliyeitwa Mdando. Baada ya kuzaliwa kwa Mdando Mhindi huyo alitishwa na kuhamia Ulaya. (Uk 160-161)

g) Ubinafsi wa Sihaba unamfanya kufungua biashara ya ukahaba. Anawatumia wasichana wadogo ili kujinufaisha. (Uk 144)

Ukatili

Hii ni tabia inayodhihirisha ukosefu wa huruma. Ukatili unatokana na moyo mgumu kiasi cha kuweza kutekeleza mauaji au kuleta hasara na mateso kwa wengine. Maudhui ya ukatili yanaendelezwa kupitia kwa Sagilu ambaye aliweza hata kuwaua washindani wake katika biashara (uk. 16). Ukatili wake unabainika pia pale anapoagiza maziwa ya watoto yenye sumu bila kujali maisha Yao.  Sagilu anapovunja ndoa za Wengine anaendeleza ukatili. Anaendeleza maudhui ya ukatili pale anapomtesa Mangwasha kimawazo huku akihatarisha ndoa yake kwa kutumia pesa kumlewesha Mrima hadi akawa mlevi na mwishowe kuachishwa kazi.

Mapenzi na asasi ya ndoa

Mapenzi ni hali ya mvuto na upendo alio nao mtu kwa mtu mwingine; hisia ya upendo aliyo nayo mtu moyoni mwake kuhusu mtu mwingine.

Ndoa ni maafikiano rasmi ya baina ya mwanamume na mwanamke ili waweze kuishi pamoja

kama mke na mume. Maudhui ya mapenzi na asasi ya ndoa yanaelezwa kupitia kwa wahusika mbalimbali. Asasi ya ndoa inakumbwa na matatizo kadha yakichangiwa na tamaa za kimwili na pesa. Hata hivyo, hakuna ndoa inayovunjika hata kama misukosuko inakuwepo. Ndoa ya Sagilu na mkewe pia inayumba pale Sagilu anapopatwa na kichaa. Mkewe anamtoroka hadi afueni inapomrejea mumewe, na ndoa hiyo kuimarika tena.

Ndoa kati ya Mrima na mkewe Mangwasha pia ina misukosuko; tokea ulevi wa Mrima na kutowajibikia ndoa yake hadi vishawishi vya pesa za Sagilu vinavyomfanya kuachishwa kazi. Uvumilivu wa angwasha mwishowe unafaulu kuokoa ndoa yake.

Mapenzi ni sehemu ya maudhui yanayojitokeza pia. Kuna mapenzi baina ya wanandoa na mapenzi baina ya vijana.

Ukiukaji wa haki za watoto

Haki ni utendaji, ufuataji na utumiaji wa sheria na kanuni katika kutimiza jambo. Maudhui ya ukiukaji wa haki za watoto yanabainika tunapomwona Mangwasha pale mwanzoni akihangaika na wanawe peke yake bila baba yao. Mrima anashiriki ulevi na maisha ya anasa hadi kuachishwa kazi.

Hajishughulishi na malezi ya wanawe kama vile kuwalisha, kuwavisha, kuwasomesha na kuwapa malezi mema kama mzazi. Anakosa uwajibikaji hadi pale anaposhurutishwa kuishi na jamaa yake na kuwajibika (uk. 1, 29, 31, 101, 115).

 

 

Nafasi ya mwanamke katika jamii

Maudhui ya nafasi ya mwanamke yanaendelezwa kupitia kwa taswira mbalimbali za mwanamke.

Mangwasha ni mwanamke aliyejikomboa kimawazo. Anakaidi mila na desturi potovu za jamii zilizopitwa na wakati pamoja na zile zinazomdhalilisha mwanamke. Tunamwona akikataa ushauri wa Chifu Mshabaha aliyetaka kumchagulia mchumba.

Anakataa ushauri wa Mbungulu pia pale anapomwambia mila hairuhusu mke kumfuata mumewe akiwa katika starehe zake (uk. 32).

Maudhui ya nafasi ya mwanamke yanajitokeza kupitia kwa Mangwasha anayejitambulisha kama mtetezi na mpiganiaji wa haki za watoto, vijana na wanaodhulumiwa katika jamii.

Mwanamke huyu akishirikiana na wengine kama Mbungulu anafaulu kuwanasua watoto wa kike waliokuwa wamenaswa katika mtego wa Sihaba aliyetaka kujitajirisha kupitia kwao.

Tunamwona pia akiwashirikisha vijana na kuwapa usaidizi wa kujiendeleza katika maisha yao.

Usaliti

Usaliti ni hali ya kwenda kinyume na matarajio ya mtu au nchi. Pia ni ile hali ya kuwafanya watu akosane kwa kuwachonganisha kupitia matumizi ya uongo.

Maudhui ya usaliti yanajitokeza kupitia kwa Chifu Mshabaha, Mrima, Sagilu, Mtemi Lesulia, Nanzia, Mbwashu na Cheiya.

Chifu Mshabaha anaisaliti jamii ya Waketwa kwa kushiriki katika njama ya kuwaondoa kutoka katika makao yao (uk. 55). Chifu anamsaliti Mangwasha anapompa Mrima bahasha ya pesa kama hongo ya kuendesha kampeni za Mtemi Lesulia (uk. 110), kinyume na matakwa ya jamii yake. Aidha, usaliti unaendelezwa na chifu pale anapomsaliti Mangwasha kwa kumleta msichana mwingine kazini kwake ili kumfuta yeye kazi (uk. 135).

Ukombozi

Ukombozi ni hali ya kumwokoa mtu au watu kutoka katika hali mbaya kama vile udhalimu au maonevu ya aina yoyote.

Maudhui ya ukombozi yanajitokeza kupitia kwa michakato ya ukombozi wa nchi ya Matuo dhidi ya uongozi mbaya wa Mtemi Lesulia na ukombozi wa Waketwa wanaodhulumiwa katika ardhi yao. Maudhui ya ukombozi yanajitokeza kupitia kwa Mangwasha anayefanya kila juhudi ya kutaka kuwakomboa Waketwa kutokana na dhuluma za utawala wa mtemi, hata kama alikuwa mwanamke asiye na cheo wala fulusi' (uk. 8).

Ijapokuwa Mangwasha hana mamlaka serikalini, anatumia nafasi yake kama mwajiriwa wa serikali katika afisi ya Chifu Mshabaha kuwaibia siri Waketwa wenzake dhidi ya njama wanazopangiwa na utawala dhalimu wa mtemi.

Uzalendo

Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake kwa dhati.

Maudhui ya uzalendo yanabainika kupitia kwa Mangwasha hasa pale inapodhihirika kuwa, "Alitamani sana kuzungumza na baadhi ya viongozi ili amani idumu nchini Matuo..." (uk. 7).

Pale anapowaibia Waketwa siri kutoka katika afisi ya Chifu Mshabaha ili kuuondoa utawala dhalimu wa mtemi ni ishara ya mwendelezo wa maudhui ya uzalendo. Mangwasha anapomkabili chifu na kumwambia kwamba serikali ni ya kila mtu bali si ya watu binafsi (uk. 136) pia ni mwendelezo wa maudhui ya uzalendo. Maudhui ya uzalendo yanasawiriwa kupitia kwa Lonare anayeepuka vifo anavyopangiwa na maadui zake ili aokoe nchi yake kutoka katika mikono ya wadhalimu. Tunaambiwa kuwa, "Alikuwa na ruwaza njema ya kusaidia wenyeji wote wa nchi ya Matuo bila ubaguzi." (uk. 10).

 

 

Elimu na ajira

Elimu ni mafunzo yanayotolewa na jamii kwa watu wake, darasani au pasipokuwa darasani.

Kwa upande mwingine, ajira ni kazi ya kulipwa mshahara.

Katika jumuiya inayozungumziwa, elimu inaonekana kukosa thamani kwa sababu hata baada ya vijana wengi kupata elimu, kazi zinagawanywa kwa kujuana. Isitoshe, kazi zinatolewa bila utaalamu wowote.

Mwandishi anasema, "Vijana wengi Waketwa waliohitimu shahada za vyuo vikuu walihangaika mijini kutafuta kazi bila mafanikio." (uk. 44). Elimu basi, inawafaidi watoto wa matajiri Wakule ambao ndio wanaofikiriwa. Hata wale wasio na ujuzi wanaajiriwa kwa misingi iyo hiyo, ndiposa maendeleo nchini yanakwama na maafa mengi kutokea. Pia anapitia masaibu kama ya Nanzia.

 

Comments

Popular posts from this blog

Nguu za Jadi - Madhari katika riwaya

Nguu za Jadi - Sifa na umuhimu wa wahusika