Nguu za Jadi - Jalada na ufaafu wa anwani

 Jalada na Ufaafu wa Anwani: Riwaya ya Nguu za Jadi

Katika jalada la riwaya ya Nguu za Jadi, kuna vitu anuwai vinavyoonekana, na vinaweza kuwa na fasiri mbalimbali kwa wasomaji tofautitofauti. Vitu vilivyopo kwenye mchoro wa jalada hilo ni:

a) Picha ya mwanamume mzee aliyeketi na anayeonekana kama anayemzungumzia mvulana. Ni wazi wamefunikwa kwa kiwango na giza. Hii inaweza kuchukuliwa kama ishara ya mtoto wa kiume ambaye ametanzwa na matatizo katika jamii ya Matuo. Mtoto wa kiume hajapewa hadhi anayostahili katika jamii hii, aidha hajawajibika inavyostahiki kama inavyoonekana baadaye kwenye riwaya yenyewe.

b) Mbele ya picha ya mwanamume anayemzungumzia mvulana kuna uwanja usiokuwa na mimea, pengine kutokana na uharibifu wa mazingira, jambo ambalo pia linajitokeza na kufanywa na viongozi na kusababisha utupu ndani ya riwaya.

c) Mbele huko kuna miti ambayo imefunikwa na giza kiasi, ambayo inaweza kuchukuliwa kuwakilisha matumaini yaliyonyimwa nafasi ya kujitokeza vizuri lakini baadaye yanashamiri hadi mwishoni mwa riwaya ambako kunafanyika uchaguzi na viongozi wawajibikaji kuchaguliwa.

d) Nyuma ya miti kuna mlima mkubwa ulio na vilele vilivyoinuka na ambavyo vina mwangaza juu. Vilele hivi ndivyo vinajulikana kama nguu.

Hii inaweza kuchukuliwa kuwa ishara ya matatizo mengi na sugu, yasiyoweza kusonga kama vile milima haiwezi kusonga au kuondolewa. Mwangaza unaoonekana juu ya vilele vya milima  unaweza kuchukuliwa kama suluhu ya  kukabiliana na nguu (vikwazo) za tangu jadi zinazotatiza maendeleo ya jamii.

e) Nyuma ya mlima kuna mwanga hafifu unaojitokeza. Mwanga huu unaweza kuchukuliwa kuwa kiwakilishi cha matumaini mapya kwamba jamii iliyokumbwa na matatizo mengi kwa muda mrefu hatimaye inapata mwanga, kama inavyofanyika kwenye riwaya Lonare anapochaguliwa kuwa mtemi, jambo linaloipa nchi ya Matuo matumaini mapya ya mabadiliko chanya.

Ufaafu wa Anwani: Nguu za Jadi

Nguu ni vilele vya milima. Katika riwaya hii, neno hili limetumiwa kisitiari, kuwakilisha vikwazo au matatizo yanayokumba jamii inayozungumziwa. Kwa hivyo, Nguu za Jadi ni vikwazo ambavyo vimekuwepo kama desturi au kanuni za maisha, na ambavyo vinadumaza maendeleo ya jamii.

 

Mifano ya vikwazo hivyo kutoka katika riwaya ni:

i. Mila ambazo zinawadunisha wanawake na kuwanyima uhuru wa kujiendeleza.

ii. Mifumo ya uongozi mbaya inayosababisha ufisadi, ukabila, utabaka, ubinafsi, hali ya kutowajibika, ufujaji wa mali za umma, uharibifu wa mazingira, ukiukaji wa haki za watoto, ukatili na wizi wa mali ya umma.

iii. Mifumo ya ubabedume uliokolea; taasubi ya kiume yenye kudhalilisha wanawake na watoto wa kike.

iv. Mila zinazomnyima mtoto wa kiume nafasi ya kujiendeleza kwa njia za kisasa. Mila hizi zimemtelekeza mtoto wa kiume kwa kutothamini elimu na maendeleo yake.

v. Umaskini uliokithiri katika jamii.

vi. Matumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

vii. Changamoto za ndoa na ukahaba.

Comments

Popular posts from this blog

Nguu za Jadi - Madhari katika riwaya

Nguu za Jadi - Dhamira ya mwandishi

Nguu za Jadi - Sifa na umuhimu wa wahusika